Header Ads

Breaking News
recent

Vigezo vya kujiunga kidato cha 5 mwaka 2018/2019; Mwanafunzi mwenye umri zaidi ya miaka 20 kutodahiliwa


Siku chache baada ya Rais wa zamani wa Tanzania Mh Benjamin Mkapa kutoa wito kwa serikali ya Rais Magufuli kuandaa mjadala wa kitaifa juu ya kujadili changamoto zinazoikumba secta ya elimu hapa Nchini ili kuinusulu kwa kuitafutia majawabu , tumeshuhudia kasi kubwa kweli kweli kutoka taasisi za elimu Nchini kushusha miongozo huku chini yenye mabadiliko kadha wa kadha juu ya mfumo wetu wa elimu .


Muongozo wa kwanza toka kauli hii ya Mh Mkapa kutoka ulitolewa na baraza la mitihani Tanzania (NECTA) ambao ulitangaza mabadiliko ya utungaji wa mitihani wa darasa la Saba kwa kubadili maswali kutoka maswali 50 kwa somo moja mpaka maswali 45 kwa kigezo kuwa mabadiliko haya yanalenga kumpa fursa mwanafunzi kujibu mwaswali 40 katika mfumo wa kuchagua ( Multiple choice) na maswali matano ya kujieleza , hii ni kwa masomo yote mpaka hesabu mtihani unakuja na majibu ya kuchagua .

Wakati tunajadili mapungufu yaliyopo katika walaka huu wa baraza la mitihani kwa namna ambavyo bado haujakidhi mabadiliko sahihi yatakayomuandaa mwanafunzi kuwa bora zaidi kuliko ilivyo sasa , ghafra serikali imetoa walaka mwingine . Kwa sasa Walaka huu umetoka Wizara ya elimu na umetolewa na kaimu katibu Mkuu wa wizara husika Mh Dr Ave Maria Semakafu ambao unalenga kutoa maelekezo ya kubadili mfumo wa udahili wa wanafunzi wa kidato cha tano hapa Nchini .

Waraka huu umetoa maelekezo Mengi lakini moja lililonishtua mimi ni hili la Mwanafunzi ambaye atakuwa anamiaka zaidi ya 20 kutopewa nafasi ya kujiunga na kidato cha tano hata kama amefaulu kwa kiwango cha juu ,yaani hata kama Mwanafunzi huyo ndio amekuwa Mwanafunzi bora kwa mwaka husika (Tanzania one) lakini akawa na miaka 21 haruhusiwi kujiunga kidato cha tano.

elimu.jpg


Ukisoma kifungu (e) cha Muongozo wa Wizara ya elimu kinasomeka hivi " Mwanafunzi atakayedahiliwa asiwe na umri zaidi ya miaka 20"

Yaani Wizara ya Elimu inashangaa kuwa kwa nature ya mazingira yetu ya elimu nchini , Mazingira ambayo asilimia kubwa ya jamii bado ziko katika mpango wa kuhamasishwa kupeleka watoto wao shule kama ilivyo jamii za wafugaji ambazo huko awali walikuwa hawaoni umuhimu wa watoto wao kupelekwa shule na sasa wameamka wameanza kuwapeleka watoto shule ,eti Mtoto wa miaka 20 au 21 kujiunga kidato cha tano kwao ni jambo lisilo la kawaida .

Hivi hawa watu ni watanzania kweli ? Unawezaje kushangaa mtoto wa miaka 20 kujiunga kidato cha tano Tanzania hii , Nchi ambayo bado changamto za elimu ni kubwa kweli kweli ? Nchi ambayo watoto wa Shule ya msingi na sekondari bado wanasafiri kwa mitumbwi kwenda shule ? Nchi ambayo bado kule Jimbo la Kwela watoto wa miaka 7 wanasafiri zaidi ya kilometa 2 kutoka kitongoji cha Mkowe kwenda kusoma kijiji cha Miangalua ? Nchi ambayo huduma za afya ni mbovu kwa kiwango ambacho kinamlazimu mtoto anayetakiwa kupata huduma za kipimo cha MRI ni sharti atoke Kule kasulu au Kakonko kigoma aje Dar es salaam ili atibiwe ? Na bado akafika Dar es salaam ambako anaweza kukaa zaidi ya miezi mitano na akawa hajapata kipimo hicho ? Kwa kuwa Mashine ya MRI imeaharibika kwa zaidi ya mwezi ? ,Wakati huo wenzake wanaendelea na Masomo ? Unashangaaje nchi ya namna hii mtoto wa Shule ya Msingi kumaliza na miaka 16 na wa kidato cha nne kumaliza na miaka 21 ?

Hivi ni kweli serikali haijuwi sababu za umbali wa shule ziliko au sababu za kuumwa au kuchelewa kuandikishwa kunaweza kumfanya Mwanafunzi huyu akamaliza shule akiwa na miaka 21 ?

Embu chukulia Mwanafunzi ameanza shule ya msingi na miaka 8 kwa kuchelewa ,kutokana na matatizo ya kifamilia na akiwa ameanza darasa la kwanza akaugua na kuahirisha masomo mwaka mmoja na akamaliza darasa la saba akiwa na miaka 16 + (Jumlisha ) Miaka Ya kidato cha kwanza mpaka cha nne na kwasababu za kuugua mwanafunzi huyu akaahirisha tena mwaka mmoja akiwa kidato cha tatu na kumaliza na miaka 21 badala ya 20 .

Mwanafunzi huyo aliyemaliza kidato cha nne akiwa na miaka 21 anafaulu vizuri kwa kupata daraja la kwanza ( division one) . Huku akifurahia matokeo yake na furaha ya kutimiza ndoto zake za kusoma udaktari au Ualimu au fani yoyote ile kwa kwenda kitado cha tano na baadae Chuo kikuu anaambiwa kwa kuwa ana miaka 21 hapaswi kudahiliwa kidato cha tano .


Embu niambie mtoto huyu Wa kitanzania aliyesoma kwa shida anakatishwa kuendelea na masomo ya kidato cha tano kwasababu eti aliugua muda mrefu akiwa shule ya Msingi na Sekondari , Changamoto za magonjwa au za kifamilia zinamhukumu wakati changamoto hizo zilikuwa nje ya uwezo wake , chukua viatu vya mtoto huyu na uvivae uone kama utatamani kuendelea kuishi hapa Duniani.

Wizara ya elimu badala ya kuondoa vikwazo katika elimu wanaweka vikwazo zaidi hii maana yake nini , kwamba hawajui changamoto za elimu yetu au hawayajui mazingira yetu tunayoishi ? Kumbuka Viongozi wengi wanaoshiriki kutoa miongozo ya namna hii wao walisoma kidato cha tano wakiwa na miaka 24 mpaka 25 leo wanasahahu wanatunga miongozo kuzuia watoto wa wenzao kusoma kidato cha tano wakiwa na miaka 21 hivi walaka huu ungetoka wakati viongozi wetu hawa wako shuleni wangekuwa hapa walipo ?

Tulianza kuzuia watoto wetu wa kike kurudi shule baada ya kupata mimba , sasa tumekuja kuzuia watoto wenye miaka 21 kusoma kidato cha tano , hivi haya ndio mabadiliko ya kuinua elimu yetu ? Au ni mabadiliko ya kuzika kabisa elimu yetu?

No comments:

Powered by Blogger.